Tuesday, January 17, 2017

Vijana wawili wafariki dunia wakati wakipiga ‘selfie’

Vijana wawili wamefariki walipokuwa wanajipiga picha katika barabara ya reli katika mji mkuu wa India Delhi.

Kundi la vijana lilikwenda katika kituo cha reli kupiga selfie mbele ya treni zilizokuwa zinawadia.

Lakini wawili walichelewa kuondoka katika reli hiyo na treni ikawakanyaga, polisi imesema.

Utafiti mwaka uliopita umeonyesha kuwa kumeshuhudiwa vifo vingi vinavyohusisha watu kupiga Selfi India kuliko nchi nyingine yoyote.

Wasomi kutoka chuo kikuu cha Carnegie Mellon na taasisi ya mawasiliano ya Indraprastha mjini Delhi wanasema kuwa kati ya vifo 127 vinavyotokana na watu kupiga Selfie kati ya mwaka 2014 – 2015, visa 76 vimeripotiwa India.

Tukio la hivi karibuni limejulikana baada ya vyombo vya habari katika eneo hilo kutoa taarifa Jumanne.

“Wakati wa kupiga picha, waliiona treni ikija wakasongea kando. Lakini treni nyingine ilitokezea upande wa pili na walikwama katikati. Waligongwa na mojawapo ya treni hizo,” Indian Express ilimnukuu afisa wa polisi.

Afisa mmoja wa polisi wa reli ameongeza kuwa vijana hao walimkodisha mpigaji picha mtaalamu kwa kazi hiyo.

“Tumeipata kamera kutoka kwa vijana iliotumika. Mlikuwa na picha na video, Video inakaguliwa, wakati picha hizo zinathibitisha kuwa walikuwa wanaruka kutoka reli moja hadi nyengine,” Naibu kamishna wa polisi Parwaiz Ahmed ameiambia Hindustan Times.

Mwaka jana wanafunzi wawili walizama walipokuwa wanapiga selfi katika mto uliofurika katika eneo la jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh.

Na polisi mjini Mumbai imetaja maeneo 15 ambapo ‘ni hatari’ kupiga Selfie baada ya msichana wa miaka 18 kuzama baharini wakati akijipiga selfie.

No comments:

Post a Comment