Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Humphrey Polepole amesema kuna mwanasiasa mmoja ambaye hana nyenzo
yoyote za kupata taarifa za uhakika ambaye amekuwa akiwaeleza na
kuwaaminisha wananchi kuwa kuna tatizo la njaa ili kuzua taharuki.
Polepole alisema baadhi ya wanasiasa wanaotangaza baa la njaa wana lengo
la kuichonganisha Serikali na wananchi.
Pamoja na kutomtaja jina, hivi
karibuni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akiwa katika kampeni za
udiwani mjini Bukoba alikaririwa akisema, “Serikali imesema haitoi
chakula, mimi nimejadiliana na chama changu tumeona tufanye mpango wa
kuwatafutia chakula Watanzania. Hata kama ni kutoka nje ya nchi
ninaamini dunia itatusikia.”
Jana, akizungumza na waandishi wa habari
juu ya mwenendo wa Serikali ya CCM katika kipindi cha mwaka mmoja,
Polepole aliwataka wananchi kuwapuuza wanasiasa wanaoleta maneno yasiyo
sahihi na yaliyojaa upotoshaji kwa Serikali.
“Sipendi kujadili watu
hapa, lakini sielewi huyu malengo yake ni nini? Tunacho chakula na imani
ya CCM ni kujitegemea, ndiyo mwelekeo wa chama hiki,” alisema.
Alieleza
kuwa duniani kote kuna utaratibu unaofahamika bayana na kuwa baa la
njaa siyo kitu kidogo, ni jambo kubwa na nchi inapokumbwa, mkuu wa nchi
ndiye mwenye dhamana ya mwisho kutangaza.
Polepole alisema lengo la
Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanajitegemea na siyo kuwa
ombaomba..., “Lakini anatokea kiongozi mmoja anawaahidi kuwa ataenda
kuwaombea chakula cha bure.
"Imeandikwa asiyefanya kazi na asile.
Watanzania hawa wametutuma tuwawekee mazingira mazuri ili wafanye kilimo
na biashara.
“Kiongozi anayesema nitaleta chakula cha bure na watu
wasifanye kazi ni bahati mbaya sana. Imani yetu ni kubwa, Watanzania
hawa wanaona mambo haya.”
Aliwataka Watanzania kuwapuuza viongozi wa
aina hiyo aliosema wanafahamu utaratibu lakini wameamua kuleta
upotoshaji wa kutoa taarifa zisizo sahihi.
Polepole aliishukuru Serikali
kwa kufafanua vyema sakata hilo akisema kuna tani milioni 1.5 za
chakula zitakazosambazwa sehemu mbalimbali zilizokumbukwa na ukame.
Alisema Awamu ya Tano, itaendelea kuishi katika misingi yake kwa kusema
ukweli daima na fitina kwake mwiko. CHANZO MPEKUZI HIURU
No comments:
Post a Comment