WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Wazara wa Elimu Sayansi na
Telnolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) kwenda mkoani Mtwara kufanya uchunguzi ili kubaini sababu
zilizosababisha shule tisa za mwisho katika matokeo ya kidato cha pili
kutoka mkoani humo.
Pia
ameziagiza halmashauri nchini kushirikiana na Idara ya Ukaguzi ili
kuhakikisha wanawasimamia vizuri walimu jambo litakalowezesha kuboresha
ufundishaji na hatimaye kupata matokeo mazuri.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumanne, Januari 17, 2017) wakati
akizungumza na watumishi na wananchi wa mkoa wa Katavi alipowasili Ikulu
ndogo ya Mpanda kwa ajili ya kufungua duka la dawa la Bohari Kuu ya
Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda.
Kwa
mujibu wa matokeo hayo kati ya shule 10 za sekondari zilizofanya vibaya
kwenye mtihani huo, tisa zinatoka katika Mkoa wa Mtwara na moja Tanga.
Shule za Mtwara zilizofanya vibaya ni Chingungwe, Malocho, Naputa,
Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Msimbati, Salama na Lukodoka huku ya
Tanga ikiwa ni Nywelo.
“Viongozi
wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) waende Mtwara wakafuatilie kwa
kina wajue kuna nini hadi shule tisa kati ya 10 zilizofanya vibaya
katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili mwaka jana zitoke huko,” alisisitiza.
Mbali
na kuuagiza huongozi wa wizara hizo kwenda mkoani Mtwara pia Waziri
Mkuu amewataka wasimamie vizuri mikoa ambayo awali ilikuwa na matokeo
mabaya na sasa inafanya vizuri na wahakikishe shule za mikoa hiyo
hazishuki na badala yake ziendelee kupata matokeo mazuri zaidi.
Awali,
akisoma taarifa ya mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali
Mstaafu, Raphael Muhuga alisema katika matokeo ya mtihani kidato cha
pili ya mwaka jana mkoa wake ulishika nafasi ya pili kitaifa ukiongozwa
na mkoa wa Geita.
Alisema
kwa sasa wanajipanga kuhakikisha katika mitihani ya mwaka huu wanashika
nafasi ya kwanza kitaifa, hivyo alitoa wito kwa watendaji wa Idara ya
Elimu, wakuu wa shule, wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja
kuhakikisha malengo hayo yanafanikiwa.
No comments:
Post a Comment