Katika kipindi cha miezi sita ya mwaka wa Fedha 2016/17 yaani kuanzia
Julai hadi Disemba 2016, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya
kodi jumla ya shilingi trilioni 7.27 ikilinganishwa na shilingi trilioni 6.44 ambazo zilikusanywa kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2015/16.
Ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2016/17 umeongezeka kwa asilimia 12.74.
Mlinganisho wa makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2015/16 na 2016/17 ni kama ifuatavyo:
MWEZI | MWAKA 2015/16 | MWAKA 2016/17 | Ongezeko |
JULAI | 925,384.7 | 1,069,458.5 | 15.57 |
AGOSTI | 923,316.9 | 1,154.222.5 | 25.01 |
SEPTEMBA | 1,132,310.3 | 1,378,048.9 | 21.70 |
OKTOBA | 1,037,179.8 | 1,131,094.9 | 9.05 |
NOVEMBA | 1,027, 939.6 | 1,123,509.7 | 9.30 |
DISEMBA | 1,403, 189.8 | 1,414,921.8 | 0.84 |
JUMLA | 6,449,321.1 | 7,271,256.26 | 12.74 |
Jitihada mbalimbali zinafanywa ili kuhakikisha TRA inaongeza
makusanyo kwa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji, kuhimiza maadili mema
kwa watumishi, kuboresha mifumo ya ukusanyaji, kushirikiana na vyombo
vingine vya dola na wananchi katika kuziba mianya ya upotevu wa mapato
pamoja na kufuatili, kuhimiza matumizi ya mashine za kielektronik na
kuhimiza ulipaji wa kodi ya majengo.
TRA inaendelea kuhimiza wafanyabiashara wote waliosajiliwa na Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) kuwasilisha ritani za VAT kabla ya tarehe 20
ya kila mwezi kama ilivyobadilishwa katika Sheria ya Fedha ya 2016.
Pamoja na hayo tunawakumbusha na kuwahimiza wananchi wa Dar es Salaam
ambao hawajafanya uhakiki wa taarifa za Namba ya Utambulisho wa
Mlipakodi (TIN) kuhakiki taarifa zao kabla ya tarehe 31 Januari 2017 ili
zoezi hilo liweze kuanzishwa katika mikoa mingine.
TRA inatoa wito kwa wafanyabiashara kulipa kodi stahiki kwa hiari na
wakati ili serikali ipate mapato yake ambayo yataiwezesha kuwahudumia
wananchi wake kikamilifu.
Kwa wafanyabiashara wenye madeni ya nyuma wanashauriwa kujitokeza
kuonana na Mameneja wa Mikoa na Wilaya kujadiliana jinsi watakavyolipa
madeni yao bila kuathiri biashara zao.
Wamiliki wa majengo wanaaswa kutoa ushirikiano kwa kulipia ankara zao za kodi ya majengo kwa hiari .
‘Pamoja Tunajenga Taifa Letu’
Richard M. Kayombo
MKURUGENZI WA HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI
No comments:
Post a Comment