Wednesday, January 18, 2017

magazeti leo tarehe18


Taarifa ya makusanyo ya kodi kwa nusu ya mwaka wa fedha 2016/17



Katika kipindi cha miezi sita ya mwaka wa Fedha 2016/17 yaani kuanzia Julai hadi Disemba 2016, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya kodi jumla ya shilingi trilioni 7.27 ikilinganishwa na shilingi trilioni 6.44 ambazo zilikusanywa kipindi kama hicho mwaka wa fedha  2015/16.
 
Ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2016/17 umeongezeka kwa asilimia 12.74.
 
Mlinganisho wa makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2015/16 na 2016/17 ni kama ifuatavyo:
MWEZI MWAKA 2015/16 MWAKA 2016/17 Ongezeko
JULAI 925,384.7 1,069,458.5 15.57
AGOSTI 923,316.9 1,154.222.5 25.01
SEPTEMBA 1,132,310.3 1,378,048.9 21.70
OKTOBA 1,037,179.8 1,131,094.9 9.05
NOVEMBA 1,027, 939.6 1,123,509.7 9.30
DISEMBA 1,403, 189.8 1,414,921.8 0.84
JUMLA 6,449,321.1 7,271,256.26 12.74

Jitihada mbalimbali zinafanywa ili kuhakikisha TRA inaongeza makusanyo kwa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji, kuhimiza maadili mema kwa watumishi, kuboresha mifumo ya ukusanyaji, kushirikiana na vyombo vingine vya dola na wananchi katika kuziba mianya ya upotevu wa mapato pamoja na kufuatili, kuhimiza matumizi ya mashine za kielektronik na kuhimiza ulipaji wa kodi ya majengo.
 
TRA inaendelea kuhimiza wafanyabiashara wote waliosajiliwa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuwasilisha ritani za VAT kabla ya tarehe 20 ya kila mwezi kama ilivyobadilishwa katika Sheria ya Fedha ya 2016.
 
Pamoja na hayo tunawakumbusha na kuwahimiza wananchi wa Dar es Salaam ambao hawajafanya uhakiki wa taarifa za Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kuhakiki taarifa zao kabla ya tarehe 31 Januari 2017 ili zoezi hilo liweze kuanzishwa katika mikoa mingine.
 
TRA inatoa wito kwa wafanyabiashara kulipa kodi stahiki kwa hiari na wakati ili serikali ipate mapato yake ambayo yataiwezesha kuwahudumia wananchi wake kikamilifu.
 
Kwa wafanyabiashara wenye madeni ya nyuma wanashauriwa kujitokeza kuonana na Mameneja wa Mikoa na Wilaya kujadiliana jinsi watakavyolipa madeni yao bila kuathiri biashara zao.
 
Wamiliki wa majengo wanaaswa kutoa ushirikiano kwa kulipia ankara zao za kodi ya majengo kwa hiari .

Pamoja Tunajenga Taifa Letu’
Richard M. Kayombo
MKURUGENZI WA HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI

Sakata la Baa la Njaa: Zitto Kabwe Atishia Kujiuzulu Ubunge Serikali Ikiwa na Tani Milioni 1.5 za Mahindi

Baada ya kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kupaza sauti kuhusu hali ya chakula nchini huku akisema kuwa serikali haina chakula cha kutosha, viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wameibuka na kusema kuwa si kweli kwamba nchi imekumbwa na njaa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Waziri wa Kilimo, Dkt Charles Tizeba ni kuwa serikali ina akiba ya chakula cha kutosheleza. Pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza juzi  mjini Dodoma aligiza Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula kusambaza chakula nchini ili kudhibiti kupanda kwa bei ya vyakula maeneo mbalimbali.

Jana kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mbunge Zitto Kabwe aliandika maneno haya;

"Serikali ya CCM ikinionyesha tani 1.5m za chakula kutoka Hifadhi ya Taifa ya Chakula ambazo inataka kusambaza najiuzulu Ubunge mara moja.
 
Narudia, mpaka Oktoba 2016 kulikuwa na nafaka tani 90,400 tu Hivi kwenye maghala yote ya NFRA.

Tunashukuru kuwa Hivi sasa ajenda ya tishio la njaa inapata majawabu na matamko. Ndio wajibu wa vyama vya siasa. Kuibua masuala muhimu kwa nchi yetu.

Nimesikia Mwenezi wa CCM ameongea na waandishi Leo. Natarajia ndugu Ado Shaibu atamkaribisha mwenzake ulingoni"- Zitto Kabwe.HABARI NA MPEKUZI HURU

Makamu Wa Rais Akutana Na Ujumbe Kutoka Kingdom Leadership Networks

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameuhimiza uongozi wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania kuharakisha mchakato wa kuanzisha Chuo cha Joseph Business School hapa nchini chuo ambacho kitatoa mafunzo mbalimbali ya biashara, maadili ya uongozi na ugunduzi wa mawazo ya biashara ili kusaidia mamia ya Watanzania kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.


Makamu wa Rais ametoa kauli ofisini kwake Ikulu Jijini Dar es Salaam leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa  Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania ambao walimtembelea Makamu wa Rais kumweleza hatua ambazo wamefikia katika uanzishaji wa Chuo hicho.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema wazo la uanzishaji wa Chuo hicho ulitolewa na Dkt Bill Winston ambaye ni Mwanzilishi wa Winston Ministries mwaka jana katika Maombezi ya Taifa ambaye yeye alikuwa mgeni rasmi katika maombi hayo, anasema aliupokea kwa furaha mpango huo kwa sababu chuo hicho kitasaidia watanzania wengi kupata elimu na ujuzi wa kuimarisha biashara zao wakati taifa likielekea kwenye uchumi wa Viwanda.

Amesema hatua za uanzishwaji wa Chuo hicho hapa nchini ni fursa pekee na nzuri kwa Watanzania kujifunza ubunifu na ugunduzi katika biashara, maadili ya uongozi katika biashara ili kuongeza ufanisi katika biashara zao kwa ajili ya manufaa yao na taifa kwa ujumla hasa katika ulipaji wa kodi.
 
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania Ibrahimu Kaduma na Meneja Mradi Dkt Charles Sokile wamemhakikishia Makamu wa Rais kuwa hatua ambazo wamefikia kwa sasa katika uanzishaji wa Chuo hicho ni nzuri ambapo mpaka sasa wamepata majengo kwa ajili ya ofisi na maeneo ya kufundishia na hatua za usajili wa chuo hicho zipo katika hatua za mwisho.

Tuesday, January 17, 2017

Mwanamke Ajinyonga Kwa Mtandio Jijini Mwanza


Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Anastazia Francis miaka 48 amekutwa akiwa amejinyonga hadi kufa katika mtaa wa Nyasaka wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.

Taarifa ya jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza imesema kuwa mnamo tarehe 16.01.2016 majira ya saa 11:00 asubuhi, mwanamke huyo alikutwa akiwa amejinyonga hadi kufa ndani ya chumba chake kwa kutumia mtandio ambao alikuwa ameuning’iniza kwenye dirisha juu.

Inadaiwa kuwa mwanamke huyo baada ya mumewe kuondoka alimtuma mwanae mkubwa aliyemaliza kidato cha nne aende dukani na mwingine mdogo mwenye umri wa miaka 06 aende kufagia na ndipo alipopata mwanya wa kwenda kujinyonga hadi kufa.

Tukio hilo lilijulikana baada ya mtoto wake mdogo kurudi ndani chumbani kuchukua shati na kumkuta mama yake akiwa amejining’inizi ndipo aliita watu ili waje kumsaidia.

Taarifa hiyo ya jeshi la polisi imesema kuwa upelelezi unaendelea ili kufahamu chanzo cha tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Ahmed Msangi amewaasa wananchi pindi wanapopata matatizo waombe ushauri kwa watu wengine ili kuweza kuepusha maamuzi ambayo ni hatari katika maisha yao.habari na mpekuzi huru

Rais Magufuli ateua Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,  tarehe 17 Januari, 2017 amemteua Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania.

Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma anachukua nafasi ya Mhe. Jaji Mohamed Chande Othman ambaye amestaafu.

Kabla ya kuteuliwa kushika nafasi ya Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania.

Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma atakaimu nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania mpaka hapo Mhe. Rais Magufuli atakapofanya uteuzi wa Jaji Mkuu wa Tanzania.

Uteuzi wa Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma unaanza mara moja.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

17 Januari, 2017

Vijana wawili wafariki dunia wakati wakipiga ‘selfie’

Vijana wawili wamefariki walipokuwa wanajipiga picha katika barabara ya reli katika mji mkuu wa India Delhi.

Kundi la vijana lilikwenda katika kituo cha reli kupiga selfie mbele ya treni zilizokuwa zinawadia.

Lakini wawili walichelewa kuondoka katika reli hiyo na treni ikawakanyaga, polisi imesema.

Utafiti mwaka uliopita umeonyesha kuwa kumeshuhudiwa vifo vingi vinavyohusisha watu kupiga Selfi India kuliko nchi nyingine yoyote.

Wasomi kutoka chuo kikuu cha Carnegie Mellon na taasisi ya mawasiliano ya Indraprastha mjini Delhi wanasema kuwa kati ya vifo 127 vinavyotokana na watu kupiga Selfie kati ya mwaka 2014 – 2015, visa 76 vimeripotiwa India.

Tukio la hivi karibuni limejulikana baada ya vyombo vya habari katika eneo hilo kutoa taarifa Jumanne.

“Wakati wa kupiga picha, waliiona treni ikija wakasongea kando. Lakini treni nyingine ilitokezea upande wa pili na walikwama katikati. Waligongwa na mojawapo ya treni hizo,” Indian Express ilimnukuu afisa wa polisi.

Afisa mmoja wa polisi wa reli ameongeza kuwa vijana hao walimkodisha mpigaji picha mtaalamu kwa kazi hiyo.

“Tumeipata kamera kutoka kwa vijana iliotumika. Mlikuwa na picha na video, Video inakaguliwa, wakati picha hizo zinathibitisha kuwa walikuwa wanaruka kutoka reli moja hadi nyengine,” Naibu kamishna wa polisi Parwaiz Ahmed ameiambia Hindustan Times.

Mwaka jana wanafunzi wawili walizama walipokuwa wanapiga selfi katika mto uliofurika katika eneo la jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh.

Na polisi mjini Mumbai imetaja maeneo 15 ambapo ‘ni hatari’ kupiga Selfie baada ya msichana wa miaka 18 kuzama baharini wakati akijipiga selfie.

Agizo la waziri mkuu baada ya Mtwara kufanya vibaya Matokeo Kidato Cha Pili

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Wazara wa Elimu Sayansi na Telnolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda mkoani Mtwara kufanya uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha shule tisa za mwisho katika matokeo ya kidato cha pili kutoka mkoani humo.
                                                                      
Pia ameziagiza halmashauri nchini kushirikiana na Idara ya Ukaguzi ili kuhakikisha wanawasimamia vizuri walimu jambo litakalowezesha kuboresha ufundishaji na hatimaye kupata matokeo mazuri.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumanne, Januari 17, 2017) wakati akizungumza na watumishi na wananchi wa mkoa wa Katavi alipowasili Ikulu ndogo ya Mpanda kwa ajili ya kufungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda.

Kwa mujibu wa matokeo hayo kati ya shule 10 za sekondari zilizofanya vibaya kwenye mtihani huo, tisa zinatoka katika Mkoa wa Mtwara na moja Tanga. Shule za Mtwara zilizofanya vibaya ni Chingungwe, Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Msimbati, Salama na Lukodoka  huku ya Tanga ikiwa ni Nywelo.

“Viongozi wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) waende Mtwara wakafuatilie kwa kina wajue kuna nini hadi shule tisa kati ya 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili mwaka jana zitoke huko,” alisisitiza.

Mbali na kuuagiza huongozi wa wizara hizo kwenda mkoani Mtwara pia Waziri Mkuu amewataka wasimamie vizuri mikoa ambayo awali ilikuwa na matokeo mabaya na sasa inafanya vizuri na wahakikishe shule za mikoa hiyo hazishuki na badala yake ziendelee kupata matokeo mazuri zaidi.

Awali, akisoma taarifa ya mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga alisema katika matokeo ya mtihani kidato cha pili ya mwaka jana mkoa wake ulishika nafasi ya pili kitaifa ukiongozwa na mkoa wa Geita.

Alisema kwa sasa wanajipanga kuhakikisha katika mitihani ya mwaka huu wanashika nafasi ya kwanza kitaifa, hivyo alitoa wito kwa watendaji wa Idara ya Elimu, wakuu wa shule, wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha malengo hayo yanafanikiwa.

CCM Yamvaa LOWASSA Sakata la Uhaba wa Chakula Nchini

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema kuna mwanasiasa mmoja ambaye hana nyenzo yoyote za kupata taarifa za uhakika ambaye amekuwa akiwaeleza na kuwaaminisha wananchi kuwa kuna tatizo la njaa ili kuzua taharuki. 
Polepole alisema baadhi ya wanasiasa wanaotangaza baa la njaa wana lengo la kuichonganisha Serikali na wananchi. 
Pamoja na kutomtaja jina, hivi karibuni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akiwa katika kampeni za udiwani mjini Bukoba alikaririwa akisema, “Serikali imesema haitoi chakula, mimi nimejadiliana na chama changu tumeona tufanye mpango wa kuwatafutia chakula Watanzania. Hata kama ni kutoka nje ya nchi ninaamini dunia itatusikia.” 
Jana, akizungumza na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa Serikali ya CCM katika kipindi cha mwaka mmoja, Polepole aliwataka wananchi kuwapuuza wanasiasa wanaoleta maneno yasiyo sahihi na yaliyojaa upotoshaji kwa Serikali. 
“Sipendi kujadili watu hapa, lakini sielewi huyu malengo yake ni nini? Tunacho chakula na imani ya CCM ni kujitegemea, ndiyo mwelekeo wa chama hiki,” alisema.
 Alieleza kuwa duniani kote kuna utaratibu unaofahamika bayana na kuwa baa la njaa siyo kitu kidogo, ni jambo kubwa na nchi inapokumbwa, mkuu wa nchi ndiye mwenye dhamana ya mwisho kutangaza. 
Polepole alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanajitegemea na siyo kuwa ombaomba..., “Lakini anatokea kiongozi mmoja anawaahidi kuwa ataenda kuwaombea chakula cha bure. 
"Imeandikwa asiyefanya kazi na asile. Watanzania hawa wametutuma tuwawekee mazingira mazuri ili wafanye kilimo na biashara.
“Kiongozi anayesema nitaleta chakula cha bure na watu wasifanye kazi ni bahati mbaya sana. Imani yetu ni kubwa, Watanzania hawa wanaona mambo haya.” 
Aliwataka Watanzania kuwapuuza viongozi wa aina hiyo aliosema wanafahamu utaratibu lakini wameamua kuleta upotoshaji wa kutoa taarifa zisizo sahihi. 
Polepole aliishukuru Serikali kwa kufafanua vyema sakata hilo akisema kuna tani milioni 1.5 za chakula zitakazosambazwa sehemu mbalimbali zilizokumbukwa na ukame. 
 Alisema Awamu ya Tano, itaendelea kuishi katika misingi yake kwa kusema ukweli daima na fitina kwake mwiko. CHANZO  MPEKUZI HIURU

Polisi FEKI Watatu Wakamatwa Kilimanjaro

Polisi mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na raia wema imewatia mbaroni watu watatu wanaodaiwa kujifanya ni askari wa jeshi hilo na kuwaibia wananchi fedha na mali. 
Habari zilizopatikana jana zilisema kuwa katika upekuzi uliofanywa kwenye moja ya nyumba anayoishi mmoja wa watuhumiwa hao, kulikutwa kitambulisho cha mwalimu aliyewahi kuibiwa mamilioni ya fedha akitokea benki. 
Kwa mujibu wa habari hizo, kundi la watu hao limekuwa likiendesha vitendo vyake katika maeneo ya kituo kikuu cha mabasi mjini Moshi na mitaa mbalimbali, hususan karibu na duka la Nakumatt. 
Vyanzo mbalimbali vimedokeza watuhumiwa hao huwakamata watu na kuwapekua kisha kuwatuhumu kuwa fedha walizonazo au simu vimeibwa sehemu na wao ni washukiwa wanaotafutwa. 
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa jana alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao juzi saa nane mchana katika eneo la Njoro Relini

Godbless Lema na Mkewe Kizimbani tena Leo

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Augustino Rwezile, leo, anatarajia kuwasomea hoja za awali Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na mkewe, Neema katika kesi inayowakabili ya kumtukana Mkuu wa mkoa huo, Mrisho Gambo. 
Hoja hizo ilikuwa wasomewe Novemba 15, 2016 lakini zilikwama kusomwa kutokana na Lema kuugua ghafla na Wakili wa Serikali, Elizabeth Swai kumuomba hakimu kutumia busara ya Mahakama kuisogeza mbele kesi hiyo kutokana na hali ya mbunge huyo. 
Lema bado anasota rumande kwa siku 76 tangu Novemba 2, mwaka jana baada ya kukosa dhamana katika kesi inayomkabili ya tuhuma za kutumia lugha ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli. 
Kutokana na sababu hiyo, Hakimu Rwezile pia aliahirisha kesi ya kuhamasisha maandamano ya Ukuta inayomkabili mbunge huyo na ile ya kumtumia ujumbe mfupi wa maneno Gambo unaodaiwa kuwa na matusi hadi leo. 
Katika kesi ya kuhamasisha maandamano inayomkabili Lema peke yake, shahidi ambaye ni Mkuu wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) wa Arusha, George Katabazi ataanza kutoa ushahidi wake ambao ilikuwa atoe Novemba 15.
Awali, upande wa Jamhuri ulidai utakuwa na mashahidi watano katika kesi ya kuhamaisha maandamano na upelelezi umekamilika. 

Mashahidi wengine ni ASP Damas Masawe ambaye ni (OCCID), Inspekta Adam Nyamiti, WP 6826 DC Esta Yohana na Ezekiel Denis Kwayu kutoka kitengo cha Upelelezi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam. 
Kwa upande wa kesi ya Lema na mkewe ya kumtumia ujumbe wa matusi Gambo, itaanza kusomwa maelezo ya awali ambayo nayo itakuwa tayari kwa kuanza kusikiliza baada ya upelelezi kukamilika.HABARI NAMPEKUZI HURU

Sheria mpya yazinduliwa kudhibiti ligi ya Uchina


Klabu zinazocheza Ligi Kuu ya Uchina zitaruhusiwa kuwashirikisha wachezaji watatu ambao si wachezaji wa Uchina kwa kila mchezo katika msimu ujao utakao anza mwezi machi.
Sheria mpya imepunguza idadi ya wachezaji wa nchi za nje.
Mshambuliaji wa Chelsea Diego Costa amehusishwa na uhamisho wa kuhamia Uchina kwa kitita cha pauni milioni 39 kwa mwaka.
Katika taarifa imesema sheria mpya zitaangaziwa ''uwekezaji wa kiholela''
Hapo awali sheria ya '4+1'' ukiwaondoa watalii wanne wa uraia wowote wakiongeza mchezaji mmoja wa Asia katika kikosi cha mchezo.
Timu pia zitatarajiwa kuwataja wachezaji wa China wawili wenye chini ya umri wa miaka 23 katia kikosi chao, na mchezaji mmoja mwenye umri wa miaka 23 katika kikosi cha kwanza cha wachezaji 11 na shirikisho la soka la China.
Pia kuzingatia ada ya kuwasaini wachezaji kinyume cha sheria katika uhamisho wa hivi majuzi.
Kiungo wa kati wa Chelsea Oscar na John Mikel Obi wameihamia China mwezi huu, huku mshambuliaji wa Manchester United na Machester City Carlos Tevez, aliripotiwa kuwa mchezaji anayelipwa zaidi ulimwenguni alipojiunga na Shanghai Shenhua mwezi Disemba.
Shenhua ni klabu miongoni mwa klabu itakayo kabiliawa na sheria hiyo mpya, kwani klabu hiyo inawachezaji sita ambao si raia wa uchina katika kikosi chake.
Klabu hiyo inawachezaji kama vile Tevez, mshambuliaji wa zamani wa Chelsea Demba Ba na mshambuliaji wa zamani wa Newcastle Obafemi Martins
Costa amehusishwa na uhamisho wake wa kwenda Tianjin Quanjian, aliyemsahihi kiungo wa kati Axel Witsel kwa mshahara wa zaidi ya pauni milioni 15 kwa mwaka, mwezi huu wa Januari.

Yatazame hapa matokeo ya mtihani wa Form Two 2016 na Darasa la nne 2016


Juzi January 15 2017 Baraza la mitihani Tanzania ‘NECTA’ limetangaza matokeo ya upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili ‘FTNA’2016 na matokeo ya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne SFNA2016.
Kwa urahisi unaweza kuyaona matokeo ya Form two 2016 kwenye link iliyoandikwa ‘FTNA 2016’  >>>FTNA 2016
Unaweza kuyatazama matokeo ya darasa la nne 2016 kwenye link iliyoandikwa ‘SFNA2016’ >>>SFNA2016  

Silaha Mbalimbali zakamatwa pori la vikindu

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, limekamata silaha tano na risasi 12, katika pori la vikindu, zikiwa zimetelekezwa kufuatia operesheni maalumu ya siku saba.

Operesheni hiyo ililenga kukamata magari ya wizi, majambazi, wauzaji wa dawa za kulevya, wauza gongo na makosa ya usalama barabarani.

Mbali na hilo, operesheni hiyo imefanikiwa kukusanya sh. 215,090,000,kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani kuanzia januari 13 mpaka 15, mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Simon Sirro.Amesema kuwa wamefanya operesheni hiyo katika pori la vikindu, Mkoani Pwani kufuatia ongezeko la matukio ya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Dar es salaam.

Aidha, Sirro amesema kuwa watuhumiwa 362, walikamatwa na makosa mbalimbali na kuongeza kuwa wamekamata silaha aina ya SMG moja, shortgun mbili na bastola mbili.

Hata hivyo, Sirro amesema kuwa katika operesheni hiyo imebainisha maeneo yaliyokithiri kwa matukio ya uhalifu ni Kigogo Freshi na Yombo Vituka.

Sababu Za Edward Lowassa Kukamatwa na Polisi Jana

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana alikamatwa na polisi mkoani Geita akituhumiwa kufanya mkutano bila kibali. 
Lowassa, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alikuwa njiani akitokea mkoani Kagera, ikiwa ni mwendelezo wa ziara za viongozi wa chama hicho katika kanda zake kutekeleza Operesheni Kata Funua inayohusisha mikutano ya ndani. Hata hivyo, aliachiwa jana jioni. 
Akiwa ameongozana na viongozi na makada wa Chadema, Lowassa aliingia Geita saa 9:30 alasiri na kupokewa na umati wa wananchi waliojitokeza eneo la Nyankumbu, tayari kwa safari ya kwenda kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Nkome. 
Viongozi wengine waliokuwamo kwenye msafara huo ni Profesa Mwesiga Baregu, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Hamis Mgeja, ambaye ni kada wa chama hicho. 
Msafara huo uliokuwa wa magari matano, ukisindikizwa na pikipiki na wafuasi kadhaa wa chama hicho, ulipitia makutano ya barabara mjini Geita na kukutana na magari ya polisi yaliyosheheni askari wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD), Ally Kitumbo. 
Bila kuingilia msafara huo, magari ya polisi yaliufuatilia kwa nyuma ulipokuwa ukielekea Kata ya Nkome. 
Hali ya hewa ilichafuka baada ya msafara kufika eneo la Soko Kuu wakati wananchi walipouzuia wakitaka kumsalimia Lowassa, ambaye aligombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita. 
Kiongozi huyo alilazimika kujitokeza juu ya gari lake kuwapungia na baada ya kelele za ‘njaa, njaa, njaa’ kusikika eneo hilo, Lowassa alitumia kipaza sauti kuwaomba wananchi wawe watulivu na wawaruhusu waendelee na safari yao kuwahi mkutano wa kampeni. 
“Ndugu zangu wana-Geita, natamani kuzungumza nanyi lakini sheria inanibana. Naomba muwe watulivu na mturuhusu tuendelee na msafara kuwahi mkutano wa kampeni Nkome,” alisema Lowassa. 
Askari hao wakiongozwa na OCD, walimfuata Lowassa na kumuamuru yeye na msafara wake kwenda Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano. Wakati wa kuelekea kituoni, gari lake lilitanguliwa mbele na la polisi na nyuma kulikuwa na jingine la jeshi hilo. 
Kitendo hicho kiliwafanya wananchi waliokuwa na hamu ya kumsikiliza kiongozi huyo kuongozana kwenda kituoni, jambo lililoibua taharuki na polisi kuwatawanya kwa kufyatua mabomu ya machozi.
Waandishi wapigwa
Pamoja na kuwatawanya wananchi kwa mabomu, askari hao pia waliwapiga kwa mikanda na fimbo waandishi wa habari waliokuwa wakifanya kazi yao eneo hilo. 
Hali ilivyokuwa kituoni 
Baada ya kuwasili kituoni huku polisi wakiendelea kuwazuia wananchi, Lowassa alisalia ndani ya gari lake hadi hali ilipotulia na kutakiwa kuingia kituoni. 
Ni magari mawili pekee; la Lowassa na la Profesa Baregu, yaliyoruhusiwa kuingia eneo la polisi huku viongozi wengine kama Singo Benson ambaye ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa Chadema, na Upendo Peneza (Mbunge wa Viti Maalumu), wakitakiwa kusubiri nje. 
Kitendo cha wananchi kuzidi kufurika kituoni hapo, kiliwafanya polisi kuimarisha ulinzi, wakizuia mtu yeyote kukatiza wala kusogelea eneo hilo. Licha ya kuzingira kituo cha polisi, askari walitanda barabara inayoelekea ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita ambako pia wananchi walizuiwa kukatiza. 
Lowassa apitishwa uani
Baada ya kuona wananchi wanazidi kujaa kituoni, polisi waliamua kumtoa Lowassa kupitia mlango wa nyuma na kumhamishia ofisini kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Mponjoli Mwabulambo.
 Kama ilivyokuwa Kituo cha Kikuu cha Polisi, ulinzi pia uliimarishwa eneo lote la ofisi ya RPC baada ya Lowassa kuhamishiwa huko na wananchi kupata taarifa. 
Kiongozi huyo aliyehamia Chadema akitokea CCM mwaka 2015 aliachiwa jana jioni. Kamanda Mwabulambo alisema hawakumkamata bali walizuia msafara huo kwa ajili ya usalama wake. 
Akizungumzia suala hilo, Peneza alisema huo ni muendelezo wa ukandamizaji dhidi ya viongozi wa Chadema unaofanywa na polisi mkoani Geita, akitoa mfano kitendo cha yeye kuhojiwa kwa saa kadhaa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa madai ya uchochezi alipohutubia mkutano wa hadhara na kusema nchi inakabiliwa na njaa. HABARI NA MPEKUZIHURU

Waziri Nape Kawajibu Waliobeza Diamond Platnumz Kukabidhiwa Bendera Ya Taifa.......Ridhiwan Kikwete Hajataka Kukaa Kimya, Kamjibu Tena Nape

Waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Tanzania Nape Nnauye sio kwamba hakuona maoni ya Watanzania kwenye mitandao ya kijamii baada ya yeye kumkabidhi bendera mwimbaji wa bongofleva Diamond Platnumz kwenda Gabon kwenye michuano ya Afrika.

Waziri Nape ameziona comments za Watanzania na yeye amewajibu baada ya Diamond kuhudhuria kwenda kutumbuiza kwenye mashindano hayo ya soka Afrika yanayofanyika Gabon ambapo Nape baada ya kuona imekua gumzo mitandaoni yeye kumpa Diamond bendera.

Kupitia Twitter  yake Waziri Nape alichukua picha ya Diamond akiwa na wengine wa Afrika walioziwakilisha nchi zao kwenye mashindano yao wakiwa na bendera na kuandika "Ulizeni tena kwanini nilimkabidhi bendera Diamond"                                                               
   
Kwa sababu mjadala umekua mrefu sana kupitia twitter,baada ya post ya Waziri Nape kwenye watu walioandika tena ni Mbunge Ridhiwani Kikwete ambaye ameandika: Nafikiri Waziri amepanik kutokana na mashambulizi lkn ukweli ni kuwa tunahitaji kushiriki afcon 2019     

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 16 Januari, 2017 amefanya uteuzi wa Wabunge wawili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Balozi mmoja. Wabunge walioteuliwa ni Alhaji Abdallah Majula Bulembo na Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi. Wabunge wateule hawa wataapishwa kwa taratibu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Abdallah Bulembo ndiye mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), na pia alikuwa ni mujumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kabla ya majukumu ya kuendesha kampeni za urais mwaka 2015 zilizomuingiza Rais Magufuli madarakani. Kwa upande wake Prof Kabudi, ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Sheria, lakini kilichong'arisha zaidi ni pale alipoteuliwa na Rais Kikwete kuwa mmoja kati ya wajumbe wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Katiba, iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mst. Joseph Sinde Warioba. Prof. Kabudi amekuwa mahiri katika mihadhara mbalimbali kitaifa, hasa wakati ule wa mchakato wa Katiba Mpya. Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Benedicto Martin Mashiba kuwa Balozi. Kituo cha kazi na tarehe ya kuapishwa kwa Balozi Mteule Benedicto Martin Mashiba itatangazwa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 16 Januari, 2017 amefanya uteuzi wa Wabunge wawili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Balozi mmoja.

Wabunge walioteuliwa ni Alhaji Abdallah Majula Bulembo na Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi.

Wabunge wateule hawa wataapishwa kwa taratibu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Abdallah Bulembo ndiye mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), na pia alikuwa ni mujumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kabla ya majukumu ya kuendesha kampeni za urais mwaka 2015 zilizomuingiza Rais Magufuli madarakani.

Kwa upande wake Prof Kabudi, ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Sheria, lakini kilichong'arisha zaidi ni pale alipoteuliwa na Rais Kikwete kuwa mmoja kati ya wajumbe wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Katiba, iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mst. Joseph Sinde Warioba.

Prof. Kabudi amekuwa mahiri katika mihadhara mbalimbali kitaifa, hasa wakati ule wa mchakato wa Katiba Mpya.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemteua Bw. Benedicto Martin Mashiba kuwa Balozi.

Kituo cha kazi na tarehe ya kuapishwa kwa Balozi Mteule Benedicto Martin Mashiba itatangazwa.habarimpekuzihuru

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ataja sababu vyakula kupanda bei sokoni........Asisitiza Tanzania Haijakumbwa na Baa la Njaa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema nchi haijakumbwa na baa la njaa na amewataka Watanzania kutosikiliza kampeni za upotoshwaji zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiasha kuhusu hali ya chakula kwani si za kweli bali ni za uzushi zenye lengo la  kupandisha bei za vyakula.

Amesema Serikali ndio yenye jukumu la kutoa taarifa za kuwepo kwa njaa ama kutokuwepo na kwamba taarifa zinazosambazwa za kuwepo kwa baa la njaa nchini hazina ukweli wowote na Serikali inawahakikishia wananchi kuwepo kwa usalama wa chakula.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 16, 2017) wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa Dodoma baada ya kuzindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, ambapo amesisitiza kwamba hali ya upatikanaji chakula nchini ni tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya kutolewa kwa taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu kuwepo kwa baa la njaa nchini jambo ambalo si la kweli. Amewataka wananchi kuwa watulivu na jambo hilo likitokea Serikali itatoa taarifa.

“Mwaka jana nchi ilikuwa na akiba ya chakula cha zaidi ya tani milioni tatu hali iliyopelekea baadhi ya Wabunge na wafanyabiashara kuomba kibali cha kuuza nafaka nje ya nchi, ambapo Serikali ilitoa kibali hicho baada ya kujiridhisha kuwepo kwa akiba ya kutosha ya chakula,” amesema.

Amesema baada ya kutolewa kwa kibali hicho tani milioni 1.5 ziliuzwa nje ya nchi na Kiasi cha tani milioni 1.5 zilizobaki zilihifadhiwa kama akiba ambapo tayari wameruhusu ziuzwe hapa nchini ili kupunguza kupanda kwa bei za vyakula nchini.

“Naomba wananchi msiwe na wasiwasi juu ya hali ya chakula nchini. Msisikilize kelele zinazopigwa na watu mbalimbali pamoja kwenye baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo magazeti kwani taarifa hizo si za kweli. Chakula kipo cha kutosha licha ya mvua kusuasua katika baadhi ya maeneo nchini,” amesema.

Hata hivyo Waziri Mkuu amesema kuwa kwa sasa mvua zimeanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo amewaomba wananchi kuzitumia kwa kulima mazao ya muda mfupi yanayostahimili ukame.

Waziri Mkuu amesema kwamba endapo kutatokea uhaba wa chakula nchini, Serikali itatoa utaratibu wa namna ya upatikanaji wa chakula kwa wananchi wake.
Kuhusu kupanda wa bei ya vyakula katika baadhi ya masoko amesema inatokana na kuwepo kwa uhaba wa chakula katika nchi jirani.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kwamba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, itatoa taarifa kuhusiana na hali halisi ya chakula nchini kwa sasa na pia itatoa taarifa kuhusu hali ya mvua ili Watanzania waweze kupata ukweli wa hali ilivyo.

 IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,