Wednesday, January 18, 2017

magazeti leo tarehe18


Taarifa ya makusanyo ya kodi kwa nusu ya mwaka wa fedha 2016/17



Katika kipindi cha miezi sita ya mwaka wa Fedha 2016/17 yaani kuanzia Julai hadi Disemba 2016, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya kodi jumla ya shilingi trilioni 7.27 ikilinganishwa na shilingi trilioni 6.44 ambazo zilikusanywa kipindi kama hicho mwaka wa fedha  2015/16.
 
Ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2016/17 umeongezeka kwa asilimia 12.74.
 
Mlinganisho wa makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2015/16 na 2016/17 ni kama ifuatavyo:
MWEZI MWAKA 2015/16 MWAKA 2016/17 Ongezeko
JULAI 925,384.7 1,069,458.5 15.57
AGOSTI 923,316.9 1,154.222.5 25.01
SEPTEMBA 1,132,310.3 1,378,048.9 21.70
OKTOBA 1,037,179.8 1,131,094.9 9.05
NOVEMBA 1,027, 939.6 1,123,509.7 9.30
DISEMBA 1,403, 189.8 1,414,921.8 0.84
JUMLA 6,449,321.1 7,271,256.26 12.74

Jitihada mbalimbali zinafanywa ili kuhakikisha TRA inaongeza makusanyo kwa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji, kuhimiza maadili mema kwa watumishi, kuboresha mifumo ya ukusanyaji, kushirikiana na vyombo vingine vya dola na wananchi katika kuziba mianya ya upotevu wa mapato pamoja na kufuatili, kuhimiza matumizi ya mashine za kielektronik na kuhimiza ulipaji wa kodi ya majengo.
 
TRA inaendelea kuhimiza wafanyabiashara wote waliosajiliwa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuwasilisha ritani za VAT kabla ya tarehe 20 ya kila mwezi kama ilivyobadilishwa katika Sheria ya Fedha ya 2016.
 
Pamoja na hayo tunawakumbusha na kuwahimiza wananchi wa Dar es Salaam ambao hawajafanya uhakiki wa taarifa za Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kuhakiki taarifa zao kabla ya tarehe 31 Januari 2017 ili zoezi hilo liweze kuanzishwa katika mikoa mingine.
 
TRA inatoa wito kwa wafanyabiashara kulipa kodi stahiki kwa hiari na wakati ili serikali ipate mapato yake ambayo yataiwezesha kuwahudumia wananchi wake kikamilifu.
 
Kwa wafanyabiashara wenye madeni ya nyuma wanashauriwa kujitokeza kuonana na Mameneja wa Mikoa na Wilaya kujadiliana jinsi watakavyolipa madeni yao bila kuathiri biashara zao.
 
Wamiliki wa majengo wanaaswa kutoa ushirikiano kwa kulipia ankara zao za kodi ya majengo kwa hiari .

Pamoja Tunajenga Taifa Letu’
Richard M. Kayombo
MKURUGENZI WA HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI

Sakata la Baa la Njaa: Zitto Kabwe Atishia Kujiuzulu Ubunge Serikali Ikiwa na Tani Milioni 1.5 za Mahindi

Baada ya kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kupaza sauti kuhusu hali ya chakula nchini huku akisema kuwa serikali haina chakula cha kutosha, viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wameibuka na kusema kuwa si kweli kwamba nchi imekumbwa na njaa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Waziri wa Kilimo, Dkt Charles Tizeba ni kuwa serikali ina akiba ya chakula cha kutosheleza. Pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza juzi  mjini Dodoma aligiza Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula kusambaza chakula nchini ili kudhibiti kupanda kwa bei ya vyakula maeneo mbalimbali.

Jana kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mbunge Zitto Kabwe aliandika maneno haya;

"Serikali ya CCM ikinionyesha tani 1.5m za chakula kutoka Hifadhi ya Taifa ya Chakula ambazo inataka kusambaza najiuzulu Ubunge mara moja.
 
Narudia, mpaka Oktoba 2016 kulikuwa na nafaka tani 90,400 tu Hivi kwenye maghala yote ya NFRA.

Tunashukuru kuwa Hivi sasa ajenda ya tishio la njaa inapata majawabu na matamko. Ndio wajibu wa vyama vya siasa. Kuibua masuala muhimu kwa nchi yetu.

Nimesikia Mwenezi wa CCM ameongea na waandishi Leo. Natarajia ndugu Ado Shaibu atamkaribisha mwenzake ulingoni"- Zitto Kabwe.HABARI NA MPEKUZI HURU

Makamu Wa Rais Akutana Na Ujumbe Kutoka Kingdom Leadership Networks

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameuhimiza uongozi wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania kuharakisha mchakato wa kuanzisha Chuo cha Joseph Business School hapa nchini chuo ambacho kitatoa mafunzo mbalimbali ya biashara, maadili ya uongozi na ugunduzi wa mawazo ya biashara ili kusaidia mamia ya Watanzania kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.


Makamu wa Rais ametoa kauli ofisini kwake Ikulu Jijini Dar es Salaam leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa  Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania ambao walimtembelea Makamu wa Rais kumweleza hatua ambazo wamefikia katika uanzishaji wa Chuo hicho.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema wazo la uanzishaji wa Chuo hicho ulitolewa na Dkt Bill Winston ambaye ni Mwanzilishi wa Winston Ministries mwaka jana katika Maombezi ya Taifa ambaye yeye alikuwa mgeni rasmi katika maombi hayo, anasema aliupokea kwa furaha mpango huo kwa sababu chuo hicho kitasaidia watanzania wengi kupata elimu na ujuzi wa kuimarisha biashara zao wakati taifa likielekea kwenye uchumi wa Viwanda.

Amesema hatua za uanzishwaji wa Chuo hicho hapa nchini ni fursa pekee na nzuri kwa Watanzania kujifunza ubunifu na ugunduzi katika biashara, maadili ya uongozi katika biashara ili kuongeza ufanisi katika biashara zao kwa ajili ya manufaa yao na taifa kwa ujumla hasa katika ulipaji wa kodi.
 
Kwa Upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania Ibrahimu Kaduma na Meneja Mradi Dkt Charles Sokile wamemhakikishia Makamu wa Rais kuwa hatua ambazo wamefikia kwa sasa katika uanzishaji wa Chuo hicho ni nzuri ambapo mpaka sasa wamepata majengo kwa ajili ya ofisi na maeneo ya kufundishia na hatua za usajili wa chuo hicho zipo katika hatua za mwisho.

Tuesday, January 17, 2017

Mwanamke Ajinyonga Kwa Mtandio Jijini Mwanza


Mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Anastazia Francis miaka 48 amekutwa akiwa amejinyonga hadi kufa katika mtaa wa Nyasaka wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.

Taarifa ya jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza imesema kuwa mnamo tarehe 16.01.2016 majira ya saa 11:00 asubuhi, mwanamke huyo alikutwa akiwa amejinyonga hadi kufa ndani ya chumba chake kwa kutumia mtandio ambao alikuwa ameuning’iniza kwenye dirisha juu.

Inadaiwa kuwa mwanamke huyo baada ya mumewe kuondoka alimtuma mwanae mkubwa aliyemaliza kidato cha nne aende dukani na mwingine mdogo mwenye umri wa miaka 06 aende kufagia na ndipo alipopata mwanya wa kwenda kujinyonga hadi kufa.

Tukio hilo lilijulikana baada ya mtoto wake mdogo kurudi ndani chumbani kuchukua shati na kumkuta mama yake akiwa amejining’inizi ndipo aliita watu ili waje kumsaidia.

Taarifa hiyo ya jeshi la polisi imesema kuwa upelelezi unaendelea ili kufahamu chanzo cha tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Ahmed Msangi amewaasa wananchi pindi wanapopata matatizo waombe ushauri kwa watu wengine ili kuweza kuepusha maamuzi ambayo ni hatari katika maisha yao.habari na mpekuzi huru

Rais Magufuli ateua Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,  tarehe 17 Januari, 2017 amemteua Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania.

Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma anachukua nafasi ya Mhe. Jaji Mohamed Chande Othman ambaye amestaafu.

Kabla ya kuteuliwa kushika nafasi ya Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania.

Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma atakaimu nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania mpaka hapo Mhe. Rais Magufuli atakapofanya uteuzi wa Jaji Mkuu wa Tanzania.

Uteuzi wa Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma unaanza mara moja.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

17 Januari, 2017

Vijana wawili wafariki dunia wakati wakipiga ‘selfie’

Vijana wawili wamefariki walipokuwa wanajipiga picha katika barabara ya reli katika mji mkuu wa India Delhi.

Kundi la vijana lilikwenda katika kituo cha reli kupiga selfie mbele ya treni zilizokuwa zinawadia.

Lakini wawili walichelewa kuondoka katika reli hiyo na treni ikawakanyaga, polisi imesema.

Utafiti mwaka uliopita umeonyesha kuwa kumeshuhudiwa vifo vingi vinavyohusisha watu kupiga Selfi India kuliko nchi nyingine yoyote.

Wasomi kutoka chuo kikuu cha Carnegie Mellon na taasisi ya mawasiliano ya Indraprastha mjini Delhi wanasema kuwa kati ya vifo 127 vinavyotokana na watu kupiga Selfie kati ya mwaka 2014 – 2015, visa 76 vimeripotiwa India.

Tukio la hivi karibuni limejulikana baada ya vyombo vya habari katika eneo hilo kutoa taarifa Jumanne.

“Wakati wa kupiga picha, waliiona treni ikija wakasongea kando. Lakini treni nyingine ilitokezea upande wa pili na walikwama katikati. Waligongwa na mojawapo ya treni hizo,” Indian Express ilimnukuu afisa wa polisi.

Afisa mmoja wa polisi wa reli ameongeza kuwa vijana hao walimkodisha mpigaji picha mtaalamu kwa kazi hiyo.

“Tumeipata kamera kutoka kwa vijana iliotumika. Mlikuwa na picha na video, Video inakaguliwa, wakati picha hizo zinathibitisha kuwa walikuwa wanaruka kutoka reli moja hadi nyengine,” Naibu kamishna wa polisi Parwaiz Ahmed ameiambia Hindustan Times.

Mwaka jana wanafunzi wawili walizama walipokuwa wanapiga selfi katika mto uliofurika katika eneo la jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh.

Na polisi mjini Mumbai imetaja maeneo 15 ambapo ‘ni hatari’ kupiga Selfie baada ya msichana wa miaka 18 kuzama baharini wakati akijipiga selfie.